Tuesday, February 28, 2017

RAIS WA UEFA AIONYA MAREKANI.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Aleksander Ceferin amesema kuwa kama Marekani itweka sheria za kuzuia wageni kuingia nchini humo inaweza kuathiri maombi yao kutaka kuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026. Rais wa Marekani, Donald Trump yuko katika mchakato wa kujaribu kufungia wahamiaji kutoka nchi saba za kiislamu kutoingia nchini humo, kufuatia mahakama kuu kusimaisha zoezi hilo mara ya kwanza. Ceferin ana wasiwasi kuwa hatua kama hiyo inaweza kuwaathiri wao wenyewe katika mbio zao za kujaribu kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza toka mwaka 1994. Akizungumza na wanhabari, Ceferin amesema hatua hiyo ya Marekani ana uhakika haitawasaidia kupata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia kwasababu kama wachezaji hawataweza kwenda kwa ajili ya uamuzi wa kisiasa au vinginevyo ni wazi michuano hiyo haitaweza kuchezwa eneo hilo

JEROME VALCKE APINGA KUFUNGIWA MIAKA 10.

KATIBU mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amekata rufani kupinga adhabu ya kufungiwa miaka 10 kujishughulisha na masuala ya soka. Valcke aliyekuwa msaidizi wa karibu wa rais wa zamani wa FIFA Sepp Blatter, alifungiwa mwaka jana kwa tuhuma za kujihusisha na sakata la kujipatia fedha kwa kulangua tiketi za Kombe la Dunia. Valcke raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 56, sasa amekata rufani Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS kupinga adhabu hiyo. Mara zote Valcke amekuwa akikanusha kufanya jambo lolote kinyume cha sheria. Awali alikuwa amelimwa adhabu ya kufungiwa miaka 12 na faini ya paundi 70,800 na FIFA, ingawa baadae adhabu hiyo ilipunguzwa.

RIBERY FITI KUIVAA SCHALKE KESHO.

MENEJA wa Bayern Munich, Carlo Ancelotti amethibitisha kuwa Franck Ribery yuko fiti kwa ajili ya kuivaa Schalke 04 kesho huku kukiwa na wasiwasi wa Renato Sanches na David Alaba kukosa. Ribery hajacheza mechi yeyote toka ile waliyoshinda mabao 2-1 dhidi ya Werder Bremen Januari 28 kufuatia kupata majeruhi ya msuli, lakini alikuwepo benchi la wachezaji wa akiba wakati Bayern ilipoibugiza Hamburg mabao 8-0 Jumamosi iliyopita. Bayern wanakabiliwa na ratiba ngumu katika wiki ya kwanza ya Machi, kwnai mchezo wao war obo fainali ya DFB-Pokal itafuatiwa na safari ya mchezo wa Bundesliga dhidi ya Cologne na ule wa hatua ya timu 16 bora ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal. Mechi zote hizo za Bayern zitachezwa ndani kipindi cha siku saba. Akieleza mikakati yake, Ancelotti amesema anadhani atakuwa tayari kumpumzisha Douglas Costa na kumpa nafasi Franck Ribery kwasababu tayari yuko fiti. Hata hivyo meneja huyo aliendelea kudai kuwa bado hana uhakika na Alaba aliyepata majeruhi madogo pamoja na Sanches aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi.

KLOPP AKIRI KIBARUA KUWA MASHAKANI.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amekiri kuwa mustakabali wake uko mashakani kama akishindwa kuinua kiwango cha wachezaji wake kilichoshuka katika mechi za karibuni kufuatia kipigo kizito kutoka kwa Leicester City jana. Kipigo hicho kinakuwa cha tano kwa Liverpool katika mashindano yote msimu huu, na ingawa klabu hiyo ndio pekee ambayo haijafungwa na wapinzani wanaoshikilia nafasi sita za juu, Klopp anafahamu yeye pamoja na wachezaji wake wanacheza na mustakabali wao. Akizungumza na wanahabari Klopp amesema wamekuwa wakifuatiliwa kila siku yeye pamoja na wachezaji hivyo wasipobadilika na kurejesha makali yao ni wazi mustakabali wao utakuwa mashakani. Liverpool imefungwa mechi nne ugenini msimu huu dhidi ya Burnley, Bournemouth, Hull City na Leicester wakati pia wamepoteza mechi moja ya ugenini dhidi ya Swansea City na kuwaacha katika hatari ya kushindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

MENEJA WA MUDA WA LEICESTER AJINADI BAADA YA KUSHINDA.

MENEJA wa muda wa Leicester City, Graig Shakespeare amesema yuko tayari kupewa kibarua cha kudumu baada ya kuiongoza klabu hiyo kuichapa Liverpool mabao 3-1 kwenye mchezo wake wa kwanza. Shakespeare alipewa nafasi hiyo kutoka ile ya usaidizi aliyokuwa nayo awali kufuatia kutimuliwa kwa Claudio Ranieri Alhamisi iliyopita, miezi tisa baada ya kuwasaidia kubeba taji la Ligi Kuu. Akizungumza na wanahabari waliomuuliza kuhusiana suala hilo, Shakespeare amesema anadhani yuko tayari kwa majukumu ya kudumu kuinoa klabu hiyo lakini anawaachia wamiliki waamue. Mabao mawili ya Jamie Vardy na moja ya Danny Drinkwater yalitosha kuwapata Leicester ushindi huo na kufufua matumaini yao kupigana kutoshuka daraja, huku bao la Liverpool likifungwa na kiungo Philippe Coutinho.

ZAMPARINI KUJIUZULU PALERMO.

RAIS wa Palermo, Maurizio Zamparini anatarajiwa kujiuzulu wadhifa wake huo ka klabu hiyo ya Serie A baada ya kuiongoza kwa miaka 15. Taarifa zimedai kuwa Palermo inatarajia kutangaza mbadala wake ndani ya siku 15 zijazo kufuatia timu hiyo kupata mmiliki mwingine. Katika kipindi cha miaka 15 ya Zamparini imeshuhudia makocha kadhaa wakija na kuondoka katika klabu hiyo wakiwemo 10 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Zamparini aliinunua Palermo wakati ikiwa inashiriki Serie B mwaka 2002 na kuingoza kupanda katika Serie A msimu wa 2003 na 2004. Hata hivyo, Zamparini mwenye umri wa miaka 75 anaiacha Palermo ikiwa inashikilia nafasi ya 18 katika msimamo wa ligi hiyo huku wakiwa alama saba nje ya eneo la kutoshuka daraja baada ya kucheza mechi 26.

RAIS WA FIFA AKANUSHA KUWA NA MIPANGO YA KUMNG'OA HAYATOU.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino alikuwa nchini Ghana jana na kupuuza madai kuwa anashawishi rais wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF Issa asiungwe mkono katika uchaguzi wa shirikisho hilo. Infantino alikuwa katika taifa hilo kutoka madharibi mwa Afrika ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya bara hili ambapo pia imeshuhudia akipita katika nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe na Uganda. Akiwa nchini Zimbabwe, Infantino alihudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa ya rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo Philip Chiyangwa hatua ambayo ilizua maswali mengi. Chiyangwa ambaye ni mfanyabiashara pia alitumia mwanya huo kusherekea kuchaguliwa kwake kuongoza Baraza la Michezo la nchi za Kusini mwa Afrika-COSAFA na kuwaalika viongozi kadhaa wa soka ambao hawamuungi mkono Hayatou. Hayatou ambaye anatarajiwa kugombea kipindi kingine cha nane katika uchaguzi utakaofanyika Machi mwaka huu, anatarajiwa kupata upinzani kutoka kwa rais wa Shirikisho la Soka la Madagascar Ahmad Ahmad ambaye meneja kampeni wake ni Chiyangwa.

Friday, February 24, 2017

SIMBA NA YANGA HAPATOSHI TAIFA.

LIGI KUU Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakaowakutanisha mahasimu timu za Simba na Yanga. Mchezo huo ambao unaotarajiwa kushuhudiwa na maelfu ya mashabiki kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi utafanyika katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam baadae leo. Simba watakaokuwa wenyeji wa mchezo huo wataingia uwanjani wakiwa vinara wa ligi wakipishana na wapinzani wao Yanga wenye mchezo mmoja mkononi kwa tofauti ya alama moja. Simba waliokuwa wameweka kambi yao ya maandalizi huko Pemba wametua jijini mapema jana huku wakijinasibu kuibuka na ushindi katika mchezo huo wakati wapinzani wao waliokuwa wameweka kambi yao nje kidogo ya mji huko Kimbiji nao wakitoa majigambo yanayofanana. Mwamuzi katika mchezo huo anatarajiwa kuwa Methew Akram kutoka Mwanza atakayesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Hassan Zani wa Arusha watakaoshika vibendera. Uhuru FM itawatangazia pambano hili la watani wa jadi moja kwa moja kutoka Uwanja wa Taifa hivyo usikose kusikiliza.

MKHITARYAN KUIKOSA FAINALI YA EFL.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amethibitisha kuwa Henrikh Mkhitaryan hatarajiwi kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wao wa fainali ya Kombe la EFL dhidi ya Southampton kesho. Hata hivyo, nahodha Rooney anatarajiwa kuwepo katika kikosi hicho kufuatia nyota huyo kutoa taarifa kuwa anataka kuendelea kuitumikia United Alhamisi iliyopita. Akizungumza na wanahabari, Mourinho amesema kiungo Michael Carrick atakuwepo katika kikosi chake lakini Mkhitaryan hatakuwepo baada ya kupata majeruhi katika mchezo wa Europa League dhidi ya Saint-Etienne Jumatano iliyopita. United watavaana na Southampton wakati wakiwania kupata taji lao pili msimu huu baada ya kutwaa Ngao ya Hisani mwanzoni mwa msimu.

ROONEY AKANUSHA TETESI ZA KUTAKA KWENDA CHINA.

MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Wayne Rooney amepuuza taarifa za mazungumzo ya kwenda China na kudai kuwa bado ataendelea kubakia Old Trafford. Rooney mwenye umri wa miaka 31, amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Ligi Kuu ya China ambapo dirisha lao la usajili linafungwa Jumanne ijayo. Hata hivyo, taarifa ya nahodha huyo iliyotolewa na United imedai kuwa hana mpango wowote wa kuondoka Old Trafford msimu huu. Rooney amesema pamoja na kuwindwa na klabu zingine jambo ambalo anashukuru, ameamua kumaliza uvumi huo na kuongeza kuwa ataendelea kubakia United.

KINA SAMATTA WAPANGWA WENYEWE KWA WENYEWE EUROPA LEAGUE.

RATIBA ya michuano ya Europa League hatua ya 16 bora imepangwa mapema leo huku klabu ya KRC Genk anayocheza mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta ikipangwa kucheza na Gent zote kutoka Ubelgiji. Genk ilitinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Astra Giurgiu ya Romania kwa jumla ya mabao 3-2 katika mechi mbili walikutana katika hatua ya 32 bora. Samatta alifanikiwa kucheza mechi zote mbili kw dakika zote akiisaidia timu yake ya Genk kutoka sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Astra kabla ya kuja kushinda bao 1-0 jana nyumbani. Timu zingine katika ratiba hiyo ni Manchester United waliopangwa kucheza na Rostov FC ya Urusi, Schalke 04 watapambana na Borussia Monchengladbach zote za Ujerumani huku Celta Vigo ya Hispania wao wakivaana na FC Krasnodar ya Urusi. Wengine ni Apoel Nicosia ya Cyprus watavaana na Anderlecht ya Ubelgiji, Lyon ya Ufaransa watacheza na AS Roma ya Italia, Olympiakos ya Ugiriki dhidi ya Besiktas ya Uturuki na FC Copenhagen ya Denmark watachuana na Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Mechi za mkondo wa kwanza za michuano hiyo zinatarajiwa kuchezwa Machi 9 huku zile za marudiano zikichezwa Machi 16.

KUTIMULIWA KWA RANIERI KWAZUA GUMZO.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Leicester City, Gary Lineker amesema uamuzi wa klabu hiyo kumtimua Claudio Ranieri miezi tisa baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu, ni wa kutosamehewa. Ranieri aliiongoza klabu hiyo kutwaa taji la ligi msimu wa 2015-2016 pamoja na kupewa nafasi finyu sana ya kufanya hivyo. Leicester kwasasa inashikilia nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Kuu huku wakitolewa katika Kombe la FA na timu ya daraja la kwanza ya Millwall. Lineker ambaye aliwahi kuichezea Leicester kwa kipindi cha misimu saba, amesema baada ya yote Ranieri aliyoifanyia klabu hiyo anadhani kumtimua ni jambo lisilokubalika. Naye meneja wa zamani wa Tottenham Hotspurs, Harry Redknapp amesema hajashangazwa sana na uamuzi huo ili amesikitika kwani alifanya kazi yake vyema.

KOMBE LA DUNIA 2022 LITAACHA KUMBUKUMBU YA KUDUMU - INFANTINO.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino ana uhakika kuwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 ambayo itaandaliwa nchini Qatar itaacha kumbukumbu ya kudumu. Infantino yuko jijini Doha kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Soka ambapo kamati ya maandalizi itawasilisha mipango yake kwa ajili ya michuano hiyo. Kombe la Dunia 2022 inatarajiwa kuwa ya michuano ya mwisho kuandaliwa kwa mfumo wa sasa kama mpango wa kuongeza idadi ya washiriki kutoka 32 mpaka 48 ukipitishwa. Akizungumza na wanahabari Infantino amesema lolote litakalotokea michuano hiyo itaacha kumbukumbu ya kudumu kwasababu itafanyika Mashariki ya Kati huku ikiwa mara ya kwanza kwa nchi ya kiarabu kuwa mwenyeji. Infantino aliendelea kudai kuwa pia itakuwa mara ya kwanza michuano hiyo kuandaliwa katika majira tofauti na ilivyozoeleka jambo ambalo linayafanya kuwa ya kipekee. Rais huyo amesema michuano hiyo ya Qatar pia itakuwa muhimu kwa mashabiki kwani umbali kutoka uwanja mmoja kwenda mwingine ni chini ya saa moja.

Wednesday, February 22, 2017

DEMBELE KUENDELEA KUBAKI CELTIC.

WAKALA wa Moussa Dembele amedai kuwa nyota huyo amepanga kukataa ofa kutoka klabu kubwa Ulaya ili aweze kubaki Celtic kumalizia mkataba wake wa miaka minne. Real Madrid ndio klabu kubwa iliyotajwa hivi karibuni kumuwania Dembele ambaye amefunga mabao 27 katika mashindano yote toka ajiunge nao akitokea Fulham Juni mwaka jana. Hata hivyo, wakala wake Mamadi Fifana amesisitiza nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa bado anaatka kuendelea kuitumikia Celtic. Fifana amesema Dembele alisaini mkataba wa miaka minne hivi karibuni na amepanga kubakia hapo kwa kipindi chote hicho.

LIVERPOOL MBIONI KUUHAMA UWANJA WAO WA MAZOEZI WA MELWOOD.

KLABU ya Liverpool imetangaza mipango yake mapema leo ambayo itashuhudia kikosi chao cha kwanza kikiachana na eneo lao la kipindi kirefu la mazoezi la Melwood na kuhamia eneo jipya lililoboreshwa la Kirkby ambako ndipo akademi yao ilipo. Melwood limekuwa eneo la mazoezi kwa wachezaji kadhaa wenye majina makubwa Uingereza toka mwaka 1950, akiwemo Kenny Dalglish, Ian Rush, Robbie Fowler, John Barnes na Steven Gerrard. 
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika tovuti ya klabu hiyo, kama mpango huo ukipitishwa eneo la Melwood sasa litabadilishwa na kujengwa nyuma zipatazo 160. Ofisa mkuu wa mipango wa Liverpool, Andy Hughes amesema wanafahamu Melwood imekuwa eneo muhimu katika mafanikio na historia kubwa ya klabu hiyo. Hughes aliendelea kudai kuwa hata hivyo, eneo hilo kwasasa limekuwa dogo kulingana na mipango yao ya muda mrefu waliyokuwa nayo ndio maana wameamua kuhama na kuliendeleza kwa shughuli nyingine.

RANIERI AKITAKA KIKOSI CHAKE KUWA NA UTHUBUTU.

MENEJA wa Leicester City, Claudio Ranieri ametaka wachezaji katika kikosi chake kucheza kwa kiwango kikubwa ili kubadili upepo katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sevilla. Leicester wako alama moja juu ya eneo la kushuka daraja katika Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 25. Kutokana na kufanya hovyo katika ligi, michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ndio imekuwa pekee waliyofanya vyema msimu huu baada ya kutinga hatua ya 16 bora wakiwa vinara wa kundi lilijumuisha timu za FC Porto, FC Copenhagen na Club Brugge. Kufuatia mchezo wao huo dhidi ya Sevilla baadae leo, Ranieri amewataka wachezaji wake kuwa na uthubutu na kucheza kwa kiwango chao cha juu.

UEFA YAZIWEKA TIMU ZA REDBULL NJIA PANDA.

TAARIFA zinadai kuwa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA linatarajia kuruhusu klabu moja pekee kati ya Red Bull Salzburg na RB Leipzig kushiriki katika michuano ya aidha Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa League. Sheria za UEFA zinaeleza kuwa haitawezekana kwa klabu mbili inayomilikiwa na mdhamini, shirika au mtu mmoja, zitakazoweza kucheza michuano hiyo kwa pamoja. Kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na RB Leipzig iliyoanzishwa mwaka 2009 katika Bundesliga msimu huu wakifukuzia ubingwa na wakongwe Bayern Munich kumetoa picha ya wazi kuwa wanaweza michuano ya Ulaya msimu ujao. Kwa upande wa klabu ya Red Bull Salzburg ambao nao kama ilivyo kwa RB Leipzig nao wanadhaminiwa na kampuni ya vinywaji ya Red Bull, pia wako katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la ligi la Austria ambalo litawapa tiketi ya kufuzu michuano Ulaya. Hata hivyo, moja kati ya klabu hizo italazimika kujitoa ili kuepuka kukiuka sheria za UEFA.

CANAVARO AKIRI TIANJIN KUFANYA MAZUNGUMZO NA ROONEY.

MENEJA wa klabu ya Tianjin Quanjian ya China, Fabio Canavaro amethibitisha kuwa timu hiyo ilishafanya mazungumzo na Wayne Rooney lakini amedai hawana mpango wowote wa kendelea na mpango huo kwasababu hatafiti aina yao ya uchezaji. Nahodha huyo wa Manchester United mwenye umri wa miaka 31, alikuwa akihusishwa na tetesi za kwenda China na vyombo vya habari vya Uingereza na kumekuwa na taarifa kuwa uhamisho wake unaweza kukamilika kabla ya muda wa mwisho Februari 28. Canavaro amesema klabu ilifanya mazungumzo na Rooney pamoja na mshambuliaji Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang ambaye alikuwa na tetesi za kwenda Shanghai SIPG kwa kitita cha euro milioni 150 mwezi uliopita, lakini dili zote hizo hazipo mezani kwasasa. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kwa Rooney dili lilishindikana kutokana na nyota huyo kutokidhi kiwango cha aina ya uchezaji wao huku kwa upande wa Aubameyang wakikataliwa ofa yao na Dortmund. Tianjin walimsajili Alexandre Paton a Axel Witsel mwezi uliopita.

MALINZI AZIPONGEZA TIMU ZILIZOPANDA DARAJA.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wamezipongeza timu za Singida United na Njombe Mji kwa kufanikiwa kupanda ligi kuu msimu ujao. Rais wa TFF Jamal Malinzi amezipongeza kwa mpigo, timu za Singida United ya Singida na Njombe Mji ya Njombe kwa kupanda daraja. Juma lililopita, Rais Malinzi aliuandikia barua uongozi wa Lipuli ya Iringa kwa mafanikio ya kupanda daraja msimu huu kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/18 kama alivyofanya sasa kwa Singida United ya Singida na Njombe Mji ya Njombe. Katika salamu hizo kwa Lipuli ambayo imepanda daraja baada ya kusota miaka 17 iliposhuka daraja, Rais Malinzi alimwandikia barua Katibu Mkuu wa timu hiyo akisema: “Nitumie fursa hii kukupongeza wewe, uongozi wa klabu yako, benchi la ufundi na wadau wote wa timu ya Lipuli kufuatia kupanda daraja kwenda Ligi Kuu. Kama ilivyotokea kwa Lipuli, Rais Malinzi pia kwa moyo mkunjufu amewaandikia barua, viongozi wa Singida United ya Singida na Njombe Mji ya Njombe, akisema: “Pia nanyi nawapongeza kwa kupanda daraja. Bila shaka ni kazi kubwa imefanyika ikihusisha kujitolea kwa ari na mali kuhakikisha mnafika hapa mlipo.” Pamoja na salamu hizo za kuwapongeza, Rais Malinzi hakuacha kuziusia timu hizo akisema: “Rai yangu kwenu ni kuongeza juhudi na kuendesha klabu kwa weledi mkubwa zaidi ili muweze kuwa washindani wa kweli katika ligi (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara).”

KASEJA ATWAA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA MWEZI JANUARI.

KIPA wa timu ya Kagera Sugar, Juma Kaseja Juma amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom wa mwezi Januari kwa msimu wa 2016/2017. Kaseja aliwashinda wachezaji Mbaraka Abeid pia wa Kagera Sugar na Jamal S. Mtengeta wa Toto African. Katika mechi tatu ambazo timu ya Kagera ilicheza kwa mwezi huo, Kaseja ambaye alicheza kwa dakika zote 270 alikuwa kiongozi na mhimili wa timu na aliisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo yote ambapo ilikusanya jumla ya pointi 9 zilizoifanya timu hiyo kupanda nafasi mbili katika msimamo wa ligi kwa mwezi huo wa Januari (kutoka nafasi ya 5 hadi ya 3). Katika michezo hiyo mitatu, Kagera Sugar ilifunga mabao sita na Kaseja alifungwa bao moja tu na alionesha nidhamu ya hali ya juu ikiwemo kutopata onyo lolote (kadi). Kwa kushinda tuzo hiyo, Kaseja atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

Tuesday, February 21, 2017

ROONEY AREJEA MAZOEZINI.

MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Wayne Rooney amerejea mazoezini kuelekea mchezo wao wa marudiano dhidi ya Saint-Etienne Jumatano ijayo. Nahodha huyo wa United amekuwa nje ya uwanja kwa kile meneja Jose Mourinho alichodai majeruhi madogo ya msuli, yaliyosababisha kukosa mchezo wa mkondo wa kwanza wa michuano hiyo pamoja na ule ya Kombe la FA dhidi ya Blackburn Rovers. Mourinho amesisitiza Rooney anaweza asiwe fiti kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Saint-Etienne kwasababu ya kushindwa kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza huku pia kukiwa na hatihati ya kukosa fainali ya EFL dhidi ya Southampton Jumapili hii. Lakini nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza alirejea mazoezini mapema leo akifanya mazoezi na wenzake wengine tisa akiwemo Chris Smalling, Marcus Rashford na Henrikh Mkhitaryan.

GUARDIOLA AWASIHI NYOTA WAKE.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola anataka wachezaji wake wahimili matarajio ya mchezo wao wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Monaco licha ya kuwa anafahamu watakosolewa sana kama wakishindwa kufuzu. Meneja huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich amewahi kushinda taji la michuano hiyo mara mbili akiwa kocha na hajawahi kushindwa kufuzu nusu fainali katika mara saba alizojaribu. Akizungumza na wanahabari Guardiola amesema sio kazi rahisi kuwa hapo na anataka kuwashawishi wachezaji wake kufurahia wakati huo kwnai ni mzuri. Guardiola aliendelea kudai kuwa watu wanaweza kudhani City walitakiwa kuwa hapo lakini wanasahau kuwa klabu nyingi kubwa hazipo. Meneja huuyo amesema macho na masikio duniani kote yanawatizama na kuwachambua huku wakiwaponda kama wakifungwa na kufasifia kama wakishinda.

CLATTENBURG KUONDOKA MWISHONI MWA MSIMU.

MWAMUZI wa Ligi Kuu Mark Clattenburg anatarajiwa kuendelea na kibarua chake mpaka mwishoni mwa msimu huu. Clattenburg mwenye umri wa miaka 41, anatarajiwa kuwa mkuu wa waamuzi nchini Saudi Arabia na alitegemewa kuondoka mara moja. Hata hivyo, Ligi Kuu imethibitisha kuwa mwamuzi huyo anatarajiwa kusimamia mchezo wa Jumamosi hii kati ya West Bromwich Albion na Bournemouth katika Uwanja wa The Hawthorns. Clattenburg amekuwa mwamuzi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA toka mwaka 2006, huku akitajwa kama mmoja wa waamuzi bora duniani kwasasa. Mwaka jana alichezesha fainali tatu za michuano ya Kombe la FA, Euro 2016 na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

NIGERIA KUMUUNGA MKONO MPINZANI HAYATOU UCHAGUZI CAF.

SHIRIKISHO la Soka la Nigeria-NFF litamuunga mkono mpinzani wa rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF, Issa Hayatou katika uchanguzi ujao. Hayatou anatarajiwa kugombea kipindi cha nane lakini anakabiliwa na upinzani kutoka kwa rais wa Shirikisho la Soka la Madagascar, Ahmad Ahmad. Rais wa NFF Amaju Pinnick amesema anadhani CAF inahitaji kizazi kipya cha uongozi ili kusogeza mbele zaidi soka la bara hili. Pinnick aliendelea kudai kuwa ataendelea kufanya kazi na Hayatou kama akishinda uchaguzi lakini kwa upande wake anaona mabadiliko yanahitaji na mtu sahihi ni Ahmad. CAF inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Machi mwaka huu huko Ethiopia.

Monday, February 20, 2017

RUFANI YA NEYMAR YAKATALIWA.

MAHAKAMA ya Jinai ya Hispania imetupilia mbali rufani ya Neymar hivyo kumaanisha kuwa nyota huyo atalazimika kusimama kizimbani kujibu mashitaka dhidi ya tuhuma za rushwa zinazomkabili kutokana na uhamisho wake kutoka Santos kwenda Barcelona. Uhamisho wa nyota huyo wa kimataifa wa Brazil kwenda La Liga ulileta utata katika klabu hiyo huku Neymar, baba yake, rais wa zamani Sandro Rosell na rais wa sasa Josep Maria Bartomeu wote wakihusishwa na tuhuma hizo. Kesi hiyo iliibuliwa na kampuni moja ya Brazil ambao walidai kuwa walimnyimwa mgao wao wa asilimia 40 ya ada ya Barcelona waliyolipa kwa ajili ya nyota huyo, ambapo walidai hawakupata yote kama mkataba ulivyosema. Neymar alikata rufani kuhsuiana na kesi hiyo lakini mahakama imetupilia mbali rufani hiyo.

BARTOMEU AWAKATA MAINI MASHABIKI WALIOMZOMEA ENRIQUE.

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amesema klabu hiyo inamuunga mkono Luis Enrique kwa asilimia 100. Bartomeu amesema hakuna mpango wowote mwingine kama meneja huyo akiamua kutoongeza mkataba wake wakati utakapomalizika Juni mwaka huu. Kipigo cha mabao 4-0 walichopata Barcelona nyumbani kwa Paris Saint-Germain katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita, kimezua tetesi kuwa Enrique hataweza kuinoa klabu hiyo kwa msimu mwingine. Jorge Sampaoli na Ernesto Valverde tayari wametajwa kama makocha mabao wanaweza kuchukua nafasi kama Enrique akiondoka. Hata hivyo, Bartomeu amebainisha kuwa hawana mpango wowote mbadala kwasasa kwani kipaumbele chao ni kuhakikisha na wanafanya vizuri katika mechi zote zilizobakia msimu huu.

NYOTA WA CAMEROON ATIMIKIA CHINA.

KIUNGO wa kimataifa wa Cameroon, Christian Bassogog amejiunga na klabu ya Henan Jianye ya China akitokea Aab Fodbold ya Denmark. Mapema mwezi huu, nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 aliteuliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano kufuatia Cameroon kutwaa taji la tano la michuano ya Mataifa ya Afrika huko gabon. Klabu ya AaB ilithibitisha taarifa hizo kupitia tovuti yao huku Bassogog mwenyewe akidai alipewa ofa ambayo hawezi kuikataa. Bassogog amesema toka alipowasili kwa mara ya kwanza Aab amekuwa akifanyiwa vyema na kila mtu ndani na nje ya uwanja hivyo anawashukuru wote waliompa ushirikiano.

DANI ALVES AWAPONDA BARCELONA.

BEKI wa zamani wa Barcelona, Dani Alves amewaponda mabingwa hao wa La Liga kwa kutompa heshima aliyostahili kabla ya kuondoka kuelekea Juventus mwaka jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ametwaa maaji 23 katika msimu nane aliyokaa Camp Nou lakini aliondoka kama mchezaji huru na kujiunga na mabingwa hao wa Serie A mwaka jana. Akizungmza na wanahabari kuhusiana na hilo, Alves amesema katika kipindi cha msimu mitatu ya mwisho alikuwa akisikia tetesi za yeye kuondoka lakini uongozi hawakumwambi lolote. Alves aliendelea kudai kuwa Barcelona hawakumuheshimu kwnai walimpa ofa ya mkataba mpya baada ya kufungiwa kusajili na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Beki huyo amesema watu wanaoongoza Barcelona hajui namna na kuwajali wachezaji.

WALIOFANYA VURUGU PORT SAID WAHUKUMIWA ADHABU YA KIFO RASMI.

MAHAKAMA nchini Misri imeunga mkono adhabu za kifo dhidi ya watu 10 waliohukumiwa kufuatia vurugu zilizoua watu 74 uwanjani huko Port Said mwaka 2012. Uamuzi huo wa mahakama ya Cassation ambao ndio wa mwisho, umemuondoa mshitakiwa wa 11 ambaye hakukamatwa baada ya adhabu yake ya kifo pia kuthibitishwa na mahakama nyingine June mwaka 2015. Mahakam hiyo pia imeunga mkono kifungo cha maisha kwa watu 10 na miaka mitano kwa watu wengine 12 akiwemo ofisa wa usalama wa wakati huo wa Port Said. Uamuzi huo wa mahakama umepokelewa kwa shangwe na ndugu wa watu waliopoteza maisha katika vurugu hizo, ambao walionekana nje ya mahakama wakishangilia.

Saturday, February 18, 2017

BARCELONA INAWEZA KUBADILI MATOKEO - SUAREZ.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Luis Suarez anaamini kikosi chao kinaweza kuweka historia kwa kuwa wa kwanza kubadili matokeo ya kufungwa mabao mabao manne katika mchezo wa kwa mkondo wa kwanz wa Ligi ya Mabingwa Ulaya pindi watakaporudiana na Paris Saint-Germain Camp Nou Machi 8. Barcelona walichabangwa mabao 4-0 na mabingwa hao wa Ufaransa katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora Jumanne iliyopita na kumfanya meneja Luis Enrique kukosolewa vikali. Akizungumza na wanahabari, Suarez amesema ni vigumu kupoteza mchezo kwa idadi kubwa ya mabao lakini anakiamini kikosi chao kinaweza kubadili matokeo hayo. Suarez aliendelea kudai kuwa anafahamu itakuwa changamoto kubwa kwao lakini anaamini kwa kikosi walichonacho wanaweza kubadili chochote kama wakicheza kwa kiwango chao cha juu.

SINA MPANGO WA KURUDI BARCELONA - GUARDIOLA.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema hatarajii kurejea tena Barcelona kufuatia kuibuka mjadala wa mustakabali wa meneja wa sasa Luis Enrique baada ya timu hiyo kufanya vibaya. Enrique anatarajiwa kumaliza mkataba wake Camp Nou mwishoni mwa msim huu na nafasi ya kuondoka imeongezeka baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Paris Saint-Germain Jumanne iliyopita. Matokeo hayo katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza hatua ya 16 bora yanaiweka Barcelona katika hatari ya kutolewa kwenye michuano hiyo. Guardiola ambaye ameshinda mataji 14 katika kipindi cha miaka minne alikaa Barcelona amesema hana mpango wowote wa kurejea tena kwani kazi yake ilishakwisha.

FECAFOOT YAKANUSHA BROOS KUOMBA KIBARUA AFRIKA KUSINI.

SHIRIKISHO la Soka la Cameroon-Fecafoot limekanusha taarifa kuwa kocha wao aliyewawezesha kutwaa taji la Mataifa ya Afrika mapema mwezi huu, amekuwa na mawasiliano na viongozi wa Afrika Kusini. Mapema juzi Shirikisho la Soka la Afrika Kusini-SAFA lilimtaja Hugo Broos miongoni mwa majina yaliyotuma maombi ya kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo. Katika taarifa yao Fecafoot wamedai kuwa hakuna mawasiliano yeyote yaliyofanyika kati ya Broos na SAFA mpaka sasa. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa Broos amekuwa akipata ofa kadhaa baada ya michuano hiyo lakini hakuna yoyote waliyoitilia maanani kwani kocha huyo bado ana mkataba nao.

SPURS INAWEZA KUTWAA TAJI LA LIGI KUU.

MENEJA wa zamani wa Tottenham Hotspurs, Harry Redknapp amesema klabu hiyo itaweza kutwaa taji la Ligi Kuu ndani ya kipindi cha miaka minne. Spurs walifanikiwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha Redknapp na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali mwaka 2011. Akizungumza na wanahabari Redknapp mwenye umri wa miaka 69 amesema Spurs wamekuwa bora chini ya Mauricio Pochettino na anadhani litakuwa kosa kubwa kumuondoa kocha huyo kwasasa. Redknapp aliendelea kudai kuwa kama Spurs ikiachwa kama ilivyo anadhani katika kipindi cha miaka mitatu au minne inaweza kutwaa taji la ligi.

BELLARABI WA LEVERKUSEN AFUNGA BAO LA 50,000 BUNDESLIGA.

MSHAMBULIAJI wa Bayer Leverkusen, Karim Bellarabi amefanikiwa kufunga bao la 50,000 katika historia ya Bundesliga jana. Bellarabi alifunga bao hilo la kuongoza katika dakika ya 23 kwenye mchezo dhidi ya Augsburg likiwa ni bao lake la kwanza kwa msimu huu. Imechukua jumla ya miaka 53 kwa Bundesliga kufikia idadi hiyo ya mabao ambayo inajumuisha mabao 3,391 ya penati na mengine 984 ya kujifunga. Nguli wa Bayern Munich Gerd Muller ndio mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika ligi hiyo akiwa na mabao 365 akifuatia na Claudio Pizarro mwenye mabao 190. Katika mchezo huo Leverkusen ilishinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Augsburg, ambapo mengine yalifungwa na Javier Hernandez.

Thursday, February 16, 2017

CHIPUKIZI WA FLUMINENSE GUSTAVO SCARPA AMLIPA BECKHAM..

David Beckham Halfway Line Goal Vs Wimbldeon 1996

CLATTENBURG KUIKACHA LIGI KUU.

CHAMA cha Makocha wa Kulipwa-PGMOL kimetangaza kuwa mwamuzi Mark Clattenburg anatarajiwa kuondoka Ligi Kuu ya Uingereza na kujiunga na Shirikisho la Soka la Saudi Arabia-SAFF. Clattenburg katika miezi ya karibuni amekuwa akihusishwa na tetesi kadhaa baada ya kukiri kuwa anaweza kuondoka kama ilivyo kwa wachezaji kadhaa nyota wa Ulaya walioondoka Uingereza kufuatia ofa nono walizopewa China. Badala yake mwamuzi huyo ameamua kwenda kwenye taifa hilo la kiarabu lenye utajiri mkubwa katika soka ingawa haijathibitishwa rasmi kibarua gani haswa atapewa huko. Mwamuzi mwezake wa zamani wa Ligi kuu Howard Webb alikuwa ameteuliwa kama mkubwa wa waamuzi wa SAFF Agosti mwaka 2015 lakini mapema mwezi huu alijiuzulu kufuatia kukubali kwenda kuwa msimamizi mkuu wa shughuli za mfumo mpya wa teknologia ya video kwa ajili ya kusaidia waamuzi huko Marekani.

RAIS WA ZAMANI WA BARCELONA AMLAUMU BARTOMEU KUKIMBIA KIVULI CHAKE.

RAIS wa zamani wa Barcelona, Joan Laporta amemtuhumu rais wa sasa wa klabu hiyo Josep Maria Bartomeu kujificha kufuatia kipigo kikubwa cha fedheha walichopata kutoka kwa Paris Saint-Germain-PSG kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Barcelona walitandikwa mabao 4-0 katika Uwanja wa Parc des Princes mabao ambayo yaliwekwa kimiani na Angel Di Maria na Julian Draxler kwenye mchezo huo wa mkondo wa kwanza hatua ya 16 bora. Laporta amesema kuwa Bartomeu alitakiwa kujitokeza baada ya kipigo hicho na kukubali lawama kwa aibu hiyo waliyopata Barcelona. Laporta aliendelea kudai kuwa anafahamu kama rais lazima ujisikie vibaya na alitegemea hatua ya kwanza ambayo angechukua Bartomeu ni kujitokeza na kuzungumzia sauala hilo lakini hajamuona mahali popote. Bartomeu alichukua mikoba ya kuiongoza Barcelona Januari mwaka 2014 kufuatia kujizulu kwa Sandro Rosell na toka wakati huo klabu hiyo imefanikiwa kutwaa taji la La Liga mara mbili, Kombe la Mfalme mara mbili na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

INFANTINO ATAKA MWENYE ZAIDI YA MMOJA KOMBE LA DUNIA 2026.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Gianni Infantino amesema amepanga kuhamasisha mwenyeji zaidi ya mmoja katika Kombe la Dunia 2026 kwani michuano hiyo inaweza kugawanywa kwa nchi mpaka nne. Akizungumza na wanahabari mapema leo, Infantino amesema wanatarajia kuhamasisha kuwepo mwenyeji zaidi ya mmoja katika Kombe la Dunia kwasababu FIFA inataka kuonyesha ina busara na kufikiria mipango endelevu ya muda mrefu. Infantino aliendelea kudai kuwa wanaweza kujumuisha pamoja nchi mbili, tatu au nne ambazo zinaweza kuja na mpango wa viwanja vitatu, vinne ay vitano kila moja ili kupunguza gharama na nchi hizo zinapaswa kuwa zimepakana. Hatua hiyo inakuja kufuatia wasiwasi juu ya gharama kubwa zinazotumika michuano hiyo ikiandaliwa na nchi moja na baadae viwanja vilivyojengwa kwa fedha nyingi kutelekezwa. Michuano ya Kombe la Dunia imewahi kuandaliwa kwa ushirikiano wa nchi mbili mara moja pekee nayo ilikuwa mwaka 2002 Japan na Korea Kusini.

HATMA YA WENGER KUJULIKANA MWISHONI MWA MSIMU.

UAMUZI wa mustakabali wa meneja wa Arsenal, Arsene Wenger unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa msimu huu lakini ofa ya mkataba mpya kwa kocha huyo bado iko mezani. Pamoja na kipigo kizito walichoapata katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa 16 bora ya michuano ya Ligi ya Mabingwa jana kutoka Bayern Munich, hakuna dalili zozote za meneja huyo kutimuliwa kabla ya kumalizika kwa msimu. Inategemewa uamuzi wa kubakia au kuondoka unatarajiwa kufanyika kwa maelewano kati ya klabu na meneja huyo Mfaransa mwenye umri wa miaka 67. Wenger amekuwa meneja wa Arsenal toka mwaka 1996, na mapema msimu huu alipewa ofa ya mkataba mpya.

Tuesday, February 14, 2017

MAJERUHI YAMKOSESHA LUKAKU KAMBI DUBAI.

MSHAMBULIAJI wa Everton, Romelu Lukaku anatarajiwa kukosa kambi ya mazoezi huko Dubai kwasababu ya kupatiwa matibabu ya majeruhi ya mguu. Klabu hiyo ilitangaza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 anatarajiwa kwenda nchi kwao Ubelgiji kumuona daktari ili kushughulikia tatizo lake. Hata hivyo, Everton wana uhakika majeruhi ya Lukaku sio makubwa sana na anatarajiwa kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi kuu dhidi ya Sunderland Februari 25 mwaka huu. Mchezaji mwingine pekee aliyekosa safari hiyo ni Yannick Bolasie ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu akisumbuliwa na majeruhi ya goti. Lukaku amekua katika kiwango bora msimu huu kufuatia kufunga mabao 16 katika mechi 24 za ligi alizocheza.

RIBERY, BOATENG KUIKOSA ARSENAL KESHO.

KLABU ya Bayern Munich inatarajiwa kuwa bila winga wake Franck Ribery na beki wa kati Jerome Boateng katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal utakaofanyika kesho. Bayern walikuwa na matumaini wawili wangeweza kurejea kwa wakati kwa ajili ya mchezo huo wa mkondo wa kwanza hatua ya 16 bora utakaofanyika katika Uwanja wa Allianz Arena. Hata hivyo, inavyoonekana Ancelotti atawakosa nyota wake hao kufuatia Ribery kuwa bado anafanya mazoezi peke yake. Ribery amekuwa katika kiwango bora msimu huu akisaidia kutoa pasi za mwisho katika mechi dhidi ya Freiburg na baadae Werder Bremen kwenye ushindi wa mabao 2-1 waliopata katika mechi hizo Januari. Boateng yeye bado anaendelea kujiuguza bega lake ambalo liliteguka mwishoni mwa mwaka jana.

GUARDIOLA AMUOMBEA JESUS.

MENEJA wa Manchester City Pep Guardiola ana matumaini kuwa mshambuliaji wake Gabriel Jesus hakupata majeruhi makubwa ya mguu katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Bournemouth. Jesus mwenye umri wa miaka 19 amefunga bao katika mechi zake mbili za kwanza za ligi alizoanza lakini alijikuta akicheza dakika 14 pekee katika mchezo huo wa jana baada ya kuteguka kifundo cha mguu katika Uwanja wa Vitality. City wanatarajiwa kujua ukubwa wa tatizo alilopata Jesus baada ya kufanyiwa vipimo zaidi. Jesus ambaye alitua City akitokea Palmeiras Januari mwaka huu, alifunga bao katika ushindi waliopata dhidi ya West Ham United na Swansea City na alikuwa akitaka kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu wa klabu hiyo baada ya Emmanuel Adebayor na Kevin de Bruyne kufunga bao katika mechi zao tatu za kwanza za ligi.

BARCELONA KUFANYA USAJILI WA DHARULA KUZIBA NAFASI YA VIDAL.

MENEJA wa Barcelona, Luis Enrique amethibitisha kuwa Barcelona wanaangalia uwezekano wa kusajili beki mpya wa kulia baada ya Aleix Vidal kukosekana kwa msimu wote uliobakia. Vidal ambaye amekuwa katika kiwango kizuri toka kuanza mwaka huu aliteguka kifundo chake cha mguu katika ushindi waliopata dhidi ya Alaves Jumamosi iliyopita na anatarajiwa kukaa nje kwa miezi mitano. Kuumia huko kwa Vidal kunamuacha Sergi Roberto kuwa mchezaji pekee katika klabu hiyo anayecheza nafasi hiyo kwasasa. Dirisha la usajili kwasasa limeshafungwa, lakini kwa sheria za Hispania Barcelona wanaweza kuruhusiwa kufanya usajili wa dharula ili kuziba nafasi iliyo wazi. Akizungumza na wanahabari, Enrique amesema Vidal tayari ameshaanza matibabu na sasa wanaangalia uwezekano wa kusajili mchezaji mwingine kwasaabu sheria zinawaruhusu. Barcelona wanatarajiwa kuvaana na Paris Saint-Germain katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaochezwa huko Parc de Princes.

Sunday, February 12, 2017

KLOPP ADAI TIMU YEYOTE INGEM-MISS MANE.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp anaamini kila timu duniani ingeyumba bila Sadio Mane baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Senegal kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Tottenham Hotspurs jana. Mane alirejea kutoka katika majukumu ya kimataifa akiwa na Senegal na kufunga mabao hayo ambayo yameipa Liverpool ushindi wa kwanza kwa mwaka huu. Akizungumza na wanahabari Klopp amesema walikuwa wakihitaji mtu wa mwisho ambaye anafunga na Mane alifanya vyema katika mchezo huo. Klopp aliendelea kudai kuwa waliyumba kumkosa Mane Januari lakini kila timu duniani ingekuwa kama hivyo kwa kumkosa nyota huyo.

MWAMUZI BORA CLATTENBURG AIOMBA RADHI HULL CITY KWA BAO LA SANCHEZ.

BEKI wa Hull City, Andy Robertson amesema mwamuzi Mark Clattenburg amewaomba radhi kwa kuruhusu bao lenye utata la Alexis Sanchez lililoipa ushindi Arsenal wa mabao 2-0. Nyota huyo wa kimataifa wa Chile alionekana wazi akitumbukiza mpira wavuni kwa mkono katika dakika ya 34 kwenye mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Emirates kabla ya kufunga bao lingine kwa penati dakika za nyongeza. Akizungumza na wanahabari, Robertson amesema ni kweli sanchez alikuwa ameshika na wakati wakitoka katika vyumba wakati wa mapumziko mwamuzi aliwaomba radhi na kukiri halikustahili kuwa bao. Robertson aliendelea kudai kuwa kilikuwa kitendo cha haraka sana hivyo huwezi kumlaumu mwamuzi moja kwa moja. Naye meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesema baada ya mchezo pamoja na mwmauzi kufanya makosa kwa Hull lakini pia hata kwa upande wao mwamuzi alifanya maamuzi yaliwaumiza.

LUCA TONI APONDA WALIOSHAMBULIA GARI AKIWA NA RAIS WA VERONA.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Italia, Luca Toni amewaponda mashabiki walioshambulia gari lao akiwa na rais wa Verona Maurizio Setti wakati wakiwa njiani kuelekea kuangalia mchezo wa Serie B dhidi ya Avellino. Toni ambaye amewahi kuichezea Verona kwa misimu mitatu amedai kuwa gari lao lilivamiwa na watu 15 huku kioo cha upande mmoja wa gari kikidaiwa kuvunjwa. Toni na Setti walikuwa wakielekea katika Uwanja wa Partenio kwa ajili ya mchezo huo ambao Verone walifungw amabao 2-0, na nguli huyo wa zamani wa Bayern Munich na Juventus alikosoa vikali tukio hilo walilofanyiwa. Akihojiwa na Sky Sport, Toni ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Italia kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 2006, amesema Setti alikuwa amevaa skafu ya bluu hivyo anadhani mashabiki hao walidhani ni watu wa kawaida na hawakuwajua.

MOURINHO ADAI HASIFIWI INAVYOSTAHIKI.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amedai juhudi za safu yake ya ushambuliaji zingepongezwa zaidi kama mtu mwingine ndio angekuwa akiinoa klabu hiyo. United ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa hatua iliyowafanya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Watford ambayo yaliwekwa kimiani na Juan Mata na Antony Martial. Akizungumza na wanahabari, Mourinho aliwapongeza wachezaji wake kwa kiwango bora walichoonyesha na kuongeza kuwa kama angekuwa kocha mwingine lazima angepewa pongezi za juu kuliko yeye. United pamoja na kuendelea kubaki katika nafasi ya sita lakini nyuma ya alama moja kufikia eneo la kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

KNTE ANAFAA KUTWAA TUZO YA MCHEZAJI WA MWAKA - HENRY.

NGULI wa zamani wa soka wa Ufaransa, Thierry Henry amempigia chapuo kiungo wa Chelsea N’Golo Kante kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa PFA baada ya kuonyesha kiwango bora toka atue Stamford Bridge. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye aliisaidia Leicester City kutwaa taji la ligi msimu uliopita alihama King Power na kutua Chelsea kiangazi mwaka jana. Henry amesema wiki iliyopita alikwenda kwenye mazoezi ya Chelsea kumuona Eden Hazard lakini alikutana na Kante na kumgusa huku akimuuliza kama kweli ni yeye na kumfanya acheke. Henry aliendelea kudai kuwa kutokana na kiwango kikubwa anachokionyesha Kante haoni sababu kwanini asishinde tuzo hiyo.

SINA MPANGO WA KUONDOKA ARSENAL - WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesisitiza hana mpango wa kuondoka Arsenal pamoja na Ian Wright kudai kuwa kocha huyo yuko mbioni kuondoka. Mustakabali wa Wenger umekuwa ukihojiwa kufuatia vipigo mfululizo katika mechi dhidi ya Watford na Chelsea vilivyofanya kufifisha matumaini yao ya ubingwa. Hata hivyo, Arsenal ilirejesha makali yake kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Hull City mapema jana. Akizungumza na wanahabari waliohoji mustakabali wake baada ya mchezo huo, Wenger alibainisha kuwa bado ataendelea kuinoa klabu hiyo na hajafikiria suala la kuondoka kwasasa. Wenger aliendelea kudai kuwa jambo la muhimu kwasasa ni kuhakikisha wanshinda mechi zao halafu baada ya msimu kumalizika ndio wanaweza kujadili mustakabali wake.

Friday, February 10, 2017

KLOPP AWAPOZA MASHABIKI WA LIVERPOOL.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp bado ana uhakika kazi yake ni mpango wa muda mrefu, kueleka katika mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Tottenham Hotspurs Jumamosi hii. Liverpool imekuwa katika kiwango duni hivi karibuni wakiwa wamefanikiwa kupata ushindi katika mechi moja kati ya 10 walizocheza toka kuanza kwa mwaka huu. Kipigo cha hivi karibuni kilitoka kwa Hull City mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Klopp baadae alikubali lawama kwa kushuka kiwango cha timu hiyo. Liverpool sasa inashikilia nafasi ya tano katika msimamo wa ligi wakiwa nyuma ya vinara Chelsea kwa alama 13. Akizungumza na wanahabari Klopp amesema bado anaamini mipango yake ni ya muda mrefu na anafahamu kuwa jukumu lake ni kuwaongoza wachezaji katika njia sahihi.